Jumatatu 31 Agosti 2026 - 16:15
Dunia Inapaswa Kufuata Mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.)

Hawza/ Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Hemedi Jalala, ametoa wito kwa jamii duniani kufuata mafundisho ya Mtume Muhammad (s.a.w.w.), akisisitiza kuwa maisha na mwenendo wa Mtume Mtukufu vinafundisha misingi muhimu ya kujenga jamii yenye maadili, umoja, mshikamano na amani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Maulana Hemedi Jalala ameyasema hayo katika matembezi ya Zafa iliyofanyika jana, Jumapili, majira ya saa kumi jioni, Kigogo Posti, Jijini Dare es Salam, ambapo alieleza kwa kina baadhi ya mafundisho muhimu ambayo wanadamu wanapaswa kuyazingatia katika maisha yao. Mafundisho hayo ni kama ifuatavyo:

1. Tabia Njema na Maadili Yaliyo Bora

Maulana Sheikh Jalala amesema: Miongoni mwa mambo makubwa yaliyompamba Mtume Muhammad (s.a.w.w.) ni tabia njema na maadili ya hali ya juu. Akirejea kauli ya Mwenyezi Mungu katika Qur’ani Tukufu isemayo: 
«وَإِنَّكَ لَعَلَىٰ خُلُقٍ عَظِيمٍ»
Na hakika wewe una tabia tukufu.

Alisema kuwa: Mtume Mtukufu alikuwa mfano bora wa tabia njema kwa wanadamu, kwa mujibu wa Maulana Jalala, kumfuata Mtume hakupaswi kuishia katika kauli pekee, bali kunapaswa kuonekana katika mwenendo, namna ya kuwasiliana na watu, kuwaheshimu wengine na kutangamana nao kwa upole na utu.

2. Ukweli na Uaminifu: Sifa Zilizomtambulisha Mtume

Akizungumzia umuhimu wa ukweli na uaminifu, Maulana  Hemedi Jalala amesema: Mtume Muhammad (s.a.w.w.) alijulikana kwa sifa hizo hata kabla ya kupewa utume. Alieleza kuwa watu wa jamii yake walimtambua kwa majina ya “As-Swadiq Al-Amin” (Mkweli na Mwaminifu), jambo lililoonesha kiwango cha juu cha uaminifu aliokuwa nacho. Amesisitiza kuwa katika dunia ya leo, ambayo changamoto za uaminifu na ukweli zinaweza kuathiri mahusiano ya watu na jamii, ni muhimu kurejea katika mfano wa Mtume kwa kujenga maisha yanayozingatia ukweli, kutunza amana na kutekeleza wajibu kwa uadilifu.

3. Kuvumiliana na Kuheshimu Tofauti za Mitazamo

Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania, pia amesisitiza fundisho la kuvumiliana, huku akielezea kuwa; Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliwafundisha watu wenye tofauti za rai, mitazamo na mazingira kuishi pamoja kwa kuheshimiana na kushirikiana. Amesema mfano huo ulionekana wazi baada ya Mtume kuhamia Madina, ambako alikutana na watu wenye mitazamo na makundi mbalimbali, lakini aliweza kujenga mazingira ya kuishi pamoja nao na kushirikiana. Kwa hiyo, amesema jamii ya leo inapaswa kujifunza kutoka kwa Mtume kwamba tofauti za mawazo hazipaswi kuwa sababu ya chuki, migawanyiko au uhasama, bali zinaweza kushughulikiwa kwa hekima, mazungumzo na kuheshimiana.

4. Umoja wa Kiislamu na Umoja wa Kitaifa

Katika sehemu nyingine ya hotuba yake, Sheikh Mkuu huyo amesisitiza umuhimu wa umoja wa Kiislamu bila kujali tofauti za madhehebu, huku akieleza kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliweka misingi ya kuwafanya Waislamu kuwa umma wenye mshikamano. Amesema mafundisho hayo hayapaswi kubaki katika vitabu au katika maadhimisho pekee, bali yanapaswa kutekelezwa katika maisha halisi kwa kujenga udugu na ushirikiano miongoni mwa Waislamu. Aidha, amesisitiza umuhimu wa umoja wa kitaifa, huku akiwataka watu kuishi kwa kuheshimiana na kushirikiana licha ya tofauti zao, kwa kuwa umoja ni msingi muhimu wa maendeleo na ustawi wa jamii.

5. Amani: Urithi Muhimu wa Mtume kwa Ulimwengu

Maulana Sheikh Jalala pia amesisitiza umuhimu wa amani, akieleza kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.) aliweka misingi ya amani na mshikamano katika jamii. Amesema mafundisho ya Mtume yanatoa mwongozo wa namna ya kutatua tofauti na kujenga mahusiano yanayozingatia kuheshimiana na kuhifadhi utu wa mwanadamu. Kwa msingi huo, amewataka Waislamu na watu wote kwa ujumla kudumisha amani kama desturi njema waliyoachiwa na Mtume, na kutumia mafundisho yake katika kupunguza migogoro, kuimarisha mshikamano na kujenga jamii yenye utulivu.

Sheikh Jalala alihitimisha khutba yake kwa kusisitiza kuwa; kumuenzi Mtume Muhammad (s.a.w.w.) kunapaswa kuambatana na utekelezaji wa mafundisho yake katika maisha ya kila siku.

Amesema: Ukweli, uaminifu, kuvumiliana, umoja na amani ni miongoni mwa misingi inayoweza kuifanya jamii kuwa bora, hivyo maadhimisho ya kuzaliwa Mtume yanapaswa kuwa fursa ya kuhuisha mafundisho hayo na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha ya Waislamu na jamii kwa ujumla.

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha